Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi
Bei ya mafuta ya petroli, dizeli na taa, imeendelea kushuka nchini ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Taarifa hiyo ilitolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kuhusu bei kikomo za bidhaa za nishati hizo ambazo zinaanza kutumika leo nchini kote.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, bei za jumla na za rejareja za mafuta ya petroli, dizeli na taa zimeshuka ikilinganishwa na zile zilizotangazwa na mamlaka hiyo Februari 4, mwaka huu.
Ngamlagosi, alisema, bei za rejareja kwa petroli imepungua kwa Shilingi 116 kwa lita (asilimia 6.57), dizeli Sh. 145 sawa (asilimia 8.49) na mafuta ya taa Sh. 134 kwa lita (asilimia 8.08).
“Aidha, kwa kulinganisha matoleo haya mawili, bei za jumla zimepungua kama ifuatavyo; Petroli Sh 119.23 kwa lita sawa na asilimia 7.16, dizeli Sh. 147.94 kwa lita sawa na asilimia 9.21 na mafuta ya taa Sh. 136.79 kwa lita sawa na asilimia 8.80,” ilifafanua taarifa hiyo.
Bei mpya za nishati hizo kwa sasa kwa baadhi ya mikoa ya Dar es Salaam, petroli Sh. 1,652, dizeli 1,563 na mafuta ya taa Sh. 1,523, Arusha petroli Sh. 1736, dizeli 1,647 na taa Sh. 1,607 na Dodoma petroli Sh. 1,711, dizeli 1,621 na taa Sh. 1,581.
Alisema, kuendelea kushuka kwa bei za mafuta katika soko la ndani ndiyo kunachangiwa na kuendelea kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
Bei za mafuta masafi katika soko la dunia kwa nishati hizo, zimepungua kati ya Julai mwaka uliopita na Januari mwaka huu kwa petroli Dola 536 kwa tani (53%), dizeli Dola 400 kwa tani (46%) na mafuta ya taa Dola 440 kwa tani (48%).
Pia kati ya Septemba mwaka uliopita na Machi mwaka huu, bei za nishati hizo kwa soko la ndani zimepungua kwa jumla ya kiasi cha Sh 615 kwa lita kwa patroli, Sh. 528 dizeli na Sh. 517 kwa lita.







0 comments:
Post a Comment