Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza rasmi
kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwa madai ya
kukiuka katiba ya chama hicho kutokana na kukishtaki mahakamani.
Uamuzi wa Chadema umechukuliwa baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar
es Saalam jana kutengua pingamizi lililowekwa na Zitto katika kesi
aliyoifungua mahakamani kuzuia kujadiliwa na Kamati Kuu ya Chadema hadi
kesi yake ya msingi itakapomalizika.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, akizungumza na waandishi
wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema Zitto alikiuka katiba ya
chama hicho kifungu cha 8(a)(X) ya kukipeleka mahakamani.
Alisema matatizo ya wanachama yatashughulikiwa kwa mujibu wa maadili na nidhamu yaliyopo ndani ya katiba ya chama hicho.
Lissu alisema pamoja na katiba ya chama kueleza utaratibu, lakini
katika hali ya kushangaza, Zitto alikwenda mahakamani kukishtaki chama
huku akifahamu wazi kuwa endapo atashindwa atakuwa amefukuzwa uanachama.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema kifungu cha 8(a)(X), mwanachama
yeyote anapofungua kesi mahakamani dhidi ya chama, endapo atashindwa
atakuwa amejiondoa uanachama,” alisema Lissu.
“Zitto `ali-risk' mwenyewe kukipeleka chama mahakamani huku
akifahamu wazi kuwa endapo akishindwa atakuwa siyo mwanachama tena,
alishauriwa vibaya ili akiharibu chama badala yake kimezidi kuimarika
kuliko kilivyokuwa awali, matokeo yake tumemshinda na hicho kifo
kilichotabiriwa hatujakiona, tumezidi kuwa imara kuliko ilivyokuwa
awali,” alisema.
Aliongeza kuwa mahusiano kati ya chama na Zitto yalivunjika siku nyingi na walichokuwa wanasubiri ni uamuzi wa mahakama tu.
“Sisi hatuwezi kukubali kuwa na akina Yuda Eskarioti ndani ya chama
chetu, taratibu zinazotakiwa kufanywa na chama hivi sasa ni kuiandikia
barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili iwasiliane na mamlaka husika
kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema.
Alisema hatua nyingine itakayofuata mahakama itajulishwa kwamba Zitto si mwanachama tena kulingana na katiba ya chama hicho.
Lissu alisema baada ya mahakama kutoa uamuzi wa kesi aliyoifunga
Zitto, Kamati Kuu ya Chadema haina haja ya kukaa na kujadili tena suala
lake, isipokuwa Mahakama itatake notisi kuwa siyo mwanachama tena.
ZITTO ANENA
Kutokana na hali hiyo, Zitto jana alinukuliwa katika mitandao ya
kijamii (facebook na Twitter) akisema hajui lolote kuhusiana na uamuzi
uliofikiwa na mahakama na hakuwa na wito kuitwa mahakamani jana.
Alisema Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo amehamishiwa mkoani
Tabora na hivyo hakuwa na taarifa ya jaji mpya aliyepangiwa kuendesha
kesi hiyo.
“Kwa kesi ya Tegeta Escrow ilivyokuwa ingeshangaza waathirika kukaa
bila kunivuruga, bahati mbaya sana sivurugiki ni kazi tu, mwanasheria
wangu atatoa taarifa,” aliandika Zitto katika mitandao ya kijamii.
HUKUMU YA MAHAKAMA
Kabla ya Chadema kutangaza kumvua uachama Zitto, Mahakama Kuu Kanda
ya Dar es Salaam, ilitangaza kutupilia mbali na kuifuta kesi
iliyofunguliwa na Zitto dhidi ya Kamati Kuu ya Chadema, baada ya
kukubali pingamizi zilizowasilishwa na chama hicho.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Richard Mziray, baada ya kupitia hoja za pande zote mbili kuhusu pingamizi za Chadema.
Ilipofika saa 3:20 asubuhi, Jaji Mziray alisoma uamuzi huo mbele ya
wanaodaiwa kuwa wanachama wa Chadema huku upande wa Zitto ukiwa hauna
mwakilishi na alikuwapo wakili wa utetezi, Peter Kibatala.
Alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama imeona
Zitto alikosea kuifungua kesi hiyo katika Masijala Kuu ya Mahakama Kuu
badala ya Masijala ya Kanda ya Dar es Salaam ya mahakama hiyo.
Pia, Zitto hakuonyesha kwa sababu gani alifungua kesi hiyo ya madai
Mahakama Kuu badala ya Mahakama ya Hakimu Mkazi kama Sheria ya Mwenendo
wa Kesi za Madai.
Chadema kupitia mawakili wake, iliwasilisha kwa njia ya maandishi pingamizi dhidi ya kesi hiyo iliyofunguliwa na Zitto.
Katika pingamizi ya kwanza, Chadema ilidai kwamba haikuwa sahihi
kesi kufunguliwa Mahakama Kuu kwa sababu ilipaswa kufunguliwa Mahakama
ya Wilaya/ Hakimu Mkazi kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Kesi za
madai.
Pingamizi jingine ni kwamba kesi hiyo ilikosewa kufunguliwa
Mahakama Kuu, Masijala Kuu badala ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam.
Jaji alikubali pingamizi hizo kwamba ziko sahihi na kuitupilia mbali kesi hiyo.
“Mahakama inaamuru Zitto kukilipa Chadema gharama zote za kesi hii,” alisema Jaji Mziray.
Januari 2, mwaka 2014, Mahakama Kuu iliyoketi chini ya Jaji John
Utamwa, ilitoa zuio la muda kwa Kamati Kuu ya Chadema kujadili uanachama
wa Zitto katika kikao cha chake kilichofanyika Januari 3, mwaka jana.
Hata hivyo, Januari 3, mwaka 2014, mahakama hiyo ilisikiliza hoja
za mawakili wa pande zote mbili kuhusu maombi hayo mbele ya Jaji John
Utamwa.
Januari 7, mwaka 2014, mahakama hiyo pia ilitoa amri kwamba Zitto
asijadiliwe uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na
kutolewa maamuzi.
Katika kesi hiyo, Zitto alikuwa anatetewa na wakili, Albert Msando,
huku Chadema ikiwakilishwa na mawakili Lissu na Peter Kibatala.
Katika kesi ya msingi, Zitto alifungua kesi dhidi ya Baraza la
Wadhamini la chama hicho na Katibu Mkuu, Willibrod Slaa, akiiomba
mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu kujadili suala la uanachama
wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi na
mahakama hiyo.
Katika maombi yake, Zitto aliiomba mahakama kuiamuru Kamati Kuu ya
Chadema (CC) na chombo chochote kisijadili uanachama wake hadi rufaa
yake itakaposikilizwa katika Baraza Kuu la Chama.
Kadhalika, aliiomba mahakama imwamuru, Dk. Slaa kumkabidhi nakala
za taarifa na mwenendo mzima wa vikao vilivyomvua uongozi ili akate
rufaa katika ngazi ya juu ya chama hicho.
MSOMI AZUNGUMZA
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, akizungumzia hukumu hiyo
alisema Zitto ni mwanasiasa ambaye bila shaka anacheza na mifumo.
Alisema Zitto anaweza akakata rufani ngazi ya mahakama inayofuata,
ili kipindi chake cha ubunge kimalizike aweze kupata mafao yake.
Dk. Bana alisema anasikia kuna chama kinamnyemelea, hali inayoweza
kumfanya aende katika chama hicho, na kwamba wamesoma kuwa atafanya
uamuzi huo wakati wowote mwezi huu.
“Ni kijana bado, anazo njia nyingi za kuendelea kufanya siasa, kwa
kuwa taifa bado linamhitaji kama kijana mfanyasiasa za vyama vya siasa,”
alisema.
KILICHOMPONZA ZITTO
Zitto alisimamishwa Unaibu Katibu Mkuu wa Chadema na Naibu Kiongozi
Mkuu wa Upinzani Bungeni na Kamati Kuu ya Chadema sambamba na Profesa
Kitila Mkumbo, aliyesimamishwa ujumbe wa Kamati Kuu pamoja na Samson
Mwigamba, aliyesimamishwa Uenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha.
Wote walituhumiwa kuandaa waraka wa siri wa mabadiliko uliokuwa unadaiwa kutaka kufanya mapinduzi ya viongozi wakuu.







0 comments:
Post a Comment