Juhudi za kuwaokoa watu walioathiriwa na mafuriko katika sehemu kubwa ya Malawi imeanza, baada ya mafuriko mabaya kutokea nchini humo ambapo takriban watu 50 wamefariki dunia tangu mvua kubwa ilipoanza kunyesha karibu mwezi mmoja uliopita.
Mafuriko hayo, yamesababisha watu 100,000 kubaki bila makazi. Salous Chilima, Makamu wa Rais wa Malawi amesema, hali mbaya ya hewa imechelewesha operesheni za uokoaji kwa siku mbili, na kwamba helikopta zilipata shida kutua kutokana na kiwango kikubwa cha maji.
Serikali ya Malawi imepeleka jeshi na vifaa kwa kutumia helikopta na boti ili kujaribu kuwaokoa maelfu ya watu waliokwama katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo. Idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka hasa baada ya miili mingine minne kupatikana katika mto wa Shire uliokuwa umefurika kusini mwa nchi. Rais Peter Mutharika wa Malawi amesema mafuriko hayo ni janga la kitaifa na kuomba msaada wa haraka wa ndani ya nchi na kimataifa.






0 comments:
Post a Comment