Eugene Mikongoti
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeongeza muda wa mwezi mmoja kwa wanachama wake kuweza kuhakiki taarifa zao, kabla ya kuhitimisha utaratibu huo ifikapo Februari 28, mwaka huu.
Kwa mujibu wa mfuko huo, baada ya uhakiki huo, mfuko huo utaweza kuwa na data ya wanachama wake ya uhakika, taarifa zao za uhakika lakini pia kuondokana na wanachama waliopoteza sifa ya kuwa wanachama wa mfuko huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa mfuko huo, Eugene Mikongoti, alisema tangu utaratibu huo wa kujaza fomu za uhakiki kwa wanachama wake uanze Oktoba 27, mwaka jana, jumla ya wanachama 491,010 tayari wamehakikiwa sawa na asilimia 72.
“Jumla ya wanachama wetu ni 740,490 lakini lengo letu la kufanya uhakiki huu wa taarifa za mwanachama ni kupata taarifa za uhakika za mwanachama, kusafisha data lakini pia kubaini wale wote wanaonufaika na mfuko huu wakati tayari wamepoteza sifa, kama vile waliopoteza maisha na walioacha kazi,” alisema.
Alisema sababu nyingine ya uhakiki huo pamoja na kupata taarifa za wanachama za uhakika pia ni kuwezesha wanachama hao kupatiwa vitambulisho vipya vya bima vinavyotarajiwa kutolewa hivi karibuni.
Aidha, Mikongoti alisema mfuko huo umeamua kuongeza muda wa mwezi mmoja wa uhakiki wa taarifa hizo kwa wanachama wake, kutokana na ukweli kuwa katika mwezi Januari hali ya kifedha kwa watu haikuwa nzuri.
“Unajua utaratibu huu wa uhakiki unajumuisha mambo mengi, ikiwemo suala la picha kwa wategemezi, sasa wengi walishindwa kutimiza uhakiki kutokana na tatizo la kifedha, hivyo tumewaongezea muda hadi mwezi ujao ambao ndio mwisho, baada ya hapo wasiohakiki taarifa zao watashindwa kupata huduma,” alisisitiza.






0 comments:
Post a Comment