Gazeti la The EastAfrican limepigwa marufuku kusambazwa Tanzania, ikiwa ni miaka 20 baada ya kuanzishwa kwake kwa ajili ya kuandika habari za ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa barua iliyotumwa mwakilishi wa The EastAfrican nchini, uamuzi huo umechukuliwa kwa sababu gazeti hilo “limekuwa likisambazwa nchini bila ya kuwa na usajili, kinyume na kifungu cha 6 cha Sheria ya Magazeti, Namba 3 ya mwaka 1976”.
Uongozi wa Nation Media Group, ambao unamiliki gazeti la The EastAfrican, umeelezea hatua hiyo kuwa ni ya kushangaza na isiyokubalika.
Barua hiyo ya Januari 21, 2015 inaagiza kusimamishwa mara moja kwa uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo nchini Tanzania ‘’hadi litakaposajiliwa rasmi na Msajili wa Magazeti, Idara ya Habari’’.
Kabla ya kutolewa kwa barua hiyo, mwakilishi wa gazeti hilo nchini, Christopher Kidanka aliitwa Jumatano na kuhojiwa na mkurugenzi wa Idara ya Habari, ambaye pia ni msemaji wa Serikali, Assa Mwambene.
Katika mahojiano hayo, Serikali ilieleza kutofurahishwa na jinsi gazeti hilo linavyoripoti habari na uchambuzi wake (zikiwamo safu za maoni).
Mwambene alilituhumu gazeti hilo kwa kuwa na mtazamo hasi dhidi ya Tanzania. Alitoa mfano wa maoni ya hivi karibuni ambayo yalikosoa msimamo wa Serikali kuhusu waasi wa Rwanda, FDLR walioko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kama mfano wa mtazamo wa gazeti dhidi ya nchi.
Mwambene pia alielezea katuni iliyotoka kwenye toleo la wiki hii la The EastAfrican, kuwa ilionyesha kutozingatia utamaduni na kwamba ilionyesha kutomuheshimu Rais.
Matokeo yake, The EastAfrican halitakuwa likisambazwa hadi masuala ya kisheria yatakapotatuliwa.
Akizungumzia uamuzi huo wa Serikali, mwenyekiti wa Bodi ya NMG Group, Wilfred Kiboro alisema sababu zilizotolewa na Serikali zinashangaza kwa sababu gazeti hilo limekuwa likisambazwa tangu miaka 20 iliyopita.
“Kwa hakika hawawezi kuamka leo na kututangaza kuwa hatuko kihalali. Kama ingekuwa ni suala la kuweka sawa mafaili, hilo halihitaji hatua za kikatili za kufungia gazeti,” alisema.
Alisema kwamba sababu halisi “ziko sehemu nyingine “ na zinaweza tu kuhusishwa na msimamo ambao gazeti hilo, na mengine ya kampuni NMG, limechukua katika kuripoti rushwa, wizi wa mali za umma na utoaji duni wa huduma kwa watu wa Afrika Mashariki.






0 comments:
Post a Comment